Friday, 14 April 2017

KARIBU CHUO CHA AFYA AGGREY-MBEYA.


Saturday, 1 April 2017

FAHAMU: UTI, UGONJWA UNAOATHIRI MFUMO WA NJIA YA MKOJO.


UTI(Urinary tract infections) ni uambukizi wa njia ya mkojo ambao huwasumbua watu wengi siku hizi. Uambukizi huu unaweza kusababisha maumivu na kukosa raha, na ugonjwa waweza kudumu kwa siku chache kama utawahi kutibiwa kwa kutumia dawa za antibiotiki.Kuna uwezekano pia wa kuchukua hatua kuhakikisha unaepukana na maambukizi haya ya njia ya mkojo.

UTI ni ugonjwa ambao huwaathiri zaidi wanawake ukilinganisha na wanaume, na sababu kubwa ikiwa ni ya kimaumbile, ingawa kuna sababu nyingine kama kufanya ngono na historia ya kifamilia.

Watoto pia waweza kuathirika na ugonjwa huu wa UTI, husani watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka miwili na watoto wa kiume wasiotahiriwa. Dalili kuu kwa watoto wenye ugonjwa huu ni homa, ingawa vipimo huhitajika ili kuhakikisha uwepo wa ugonjwa. Wazee nao pia huweza kuathirika na
ugonjwa huu.

Mfumo wa mkojo ni ule ambao miili yetu hutengeneza na hata kuutoa mkojo nje ya mwili. Na unahusisha sehemu kuu nne:-
 • Figo(Kidney), ambazo ni ogani zilizo na umbo la haragwe na zinakuwa mbili, na ukubwa wake ni kadirio la unavyokunja ngumi yako. Kazi ya figo ni kuchuja damu na matokeo yake ni mkojo unaotengenezwa na hutolewa kama uchafu  mwilini.
 • Mirija ya kutoka figo kwenda kwenye kibofu( ureters), huwa ni miwili na hupeleka mkojo kwenda kwenye kibofu.      
 • Kibofu, ambacho kazi yake ni kukusanya na kuhifadhi mkojo unaotoka katika figo,mkojo hutolewa pale mtu anapoamua kukojoa.      
 • Mrija wa kutoa mkojo kutoka kwenye kibofu(urethra), huu ni mrija mmoja ambao hutoa mkojo nje mtu anapoamua kukojoa.

UTI husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao huingia katika mrija wa kutoa mkojo kutoka katika kibofu. Asilimia kubwa ya ugonjwa huu katika jamii husababishwa na bakteria ajulikanaye kama Escherichia coli(E Coli), Pia asilimia ndogo yaweza kusababishwa na aina nyingine ya bakteria ajulikanaye kama Staphylococcus saprophyticus.Lakini pia kwa uchache sana ugonjwa waweza kusababishwa na fangasi au virusi.

Ugonjwa huu ambao hauko katika kundi la magonjwa ya zinaa, lakini kufanya ngono wakati mwingine husababisha kuambukizwa kwa ugonjwa huu
Dalili za UTI hutofautiana kulingana na sehemu ya njia ya mkojo iliyoathirika.
Jedwali
Sehemu iliyoathirika
Dalili
Figo

 •  Kichefuchefu.
 • Kutapika.
 • Maumivu ya mgongo wa juu.
 • Homa kali.
 • Kutetemeka na kusikia baridi
Kibofu

 • Damu katika mkojo.
 • Maumivu ya nyonga.
 • Maumivu chini ya kitovu.
 • Kukojoa mara kwa mara na kupata maumivu wakati wa kukojoa.

Mrija wa kutoa mkojo kutoka kwenye kibofu (urethra)

 • Mkojo wa kuunguza wakati wa kukojoa(maumivu njia ya mkojo)

Siyo mara zote ambazo mtu hupata dalili za ungonjwa huu, lakini zinapotokea huwa ni kama ifuatavyo:- Kujisikia haja ya kukojoa mara kwa mara, kusikia maumivu wakati wa kukojoa, kukojoa mara kwa mara mkojo kidogo, mkojo wa rangi ya mawingu mawingu, mkojo mwekundu au pink, pia wa rangi ya brauni, mkojo unaotoa harufu, maumivu ya nyonga kwa wanawake na maumivu kwenye njia ya haja kubwa kwa wanaume. Endapo utakuwa na dalili hizo zilizotajwa awali ni vyema kupata ushauri wa daktari.

Uambukizi wa njia ya mkojo hutokea kama bakteria wataingia katika mrija wa kutoa mkojo kutoka katika kibofu, na huzaliana na kuongezeka katika kibofu. Ingawa bakteria hawa waweza kuishi katika kibofu bila kuleta madhara, lakini wakati mwingine kinga ya mwili hushindwa kufanya kazi ipasavyo na uambukizi hutokea. Uambukizi unapotokea ndipo mgonjwa anaweza kuona dalili mbalimbali tulizoziona awali.

Kama tulivyoona awali mara nyingi ugonjwa huu huwaathiri zaidi wanawake na sababu kubwa ikiwa ni ya maumbile.
 • Uambukizi katika mrija wa kutoa mkojo kutoka katika kibofu (Infection of the urethra)-Aina hii ya UTI hutokea endapo bakteria wanaopatikana tumboni watasambaa kutoka njia ya haja kubwa na kuingia katika mrija wa mkojo. Na kwa kuwa mrija wa kutoa mkojo uko karibu uke mwanamke anaweza pia kuambukizwa UTI kwa kufanya ngono, ambapo vijimelea kama gonococcus na chlamydia vinaweza kusabisha aina hii ya UTI.
 • Uambukizi katika kibofu- Aina hii ya UTI mara nyingi husababishwa na bakteria aina ya  E coli,  bakteria hawa hupatikana tumboni.Maumbile ya uke kuwa karibu ya njia ya aja kubwa huchangia sana bakteria hawa kuweza kuingia kwa urahisi katika njia ya mkojo na kusababisha uambukizi.


Walio katika hatari ya kupata ugonjwa.
 • Wagonjwa walioingiziwa mpira wa kusaidia kutoa mkojo(catheter) huwa katika hatari kubwa ya kupata UTI. Hii inajumuisha wagonjwa waliolazwa, wenye matatizo ya magonjwa ya fahamu na hawawezi kutoa mkojo, pia wagonjwa  waliopooza.
 • Wagonjwa walio na kinga ya mwili iliyoshuka, mfano wale wenye kisukari na magonjwa mengineo yanayoshusha kinga ya mwili dhidi ya vijimelea vya magonjwa, wanakuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huu.
 • Wagonjwa walioziba njia ya mkojo, hii inaweza kusababishwa na mawe ya kwenye figo na kukua kwa tezi dume kwa wanaume, hii husabisha mkojo wenye bakteria kushindwa kutoka na kusababisha uambukizi katika kibofu na figo.
 • Hitilafu katika njia ya mkojo- inawezekana mtoto kuzaliwa na hitilafu hii ambayo husababisha mkojo kushindwa kutoka kwa urahisi na kuchochea maambukizi haya ya UTI.
 • Ukomo wa hedhi, hii ni kwa sababu homoni ya ostrogeni hupungua na kusababisha mabadiliko katika njia ya mkojo.
 • Matumizi ya njia za uzazi wa mpango, ambayo vipandikizi huwekwa katika njia ya kizazi(diaphragm).Yaweza pia kuchochea kupata maambukizi haya.
 • Kuwa katika umri wa matamanio ya kufanya ngono. Wanawake walio katika umri wa matamanio ya ngono wameonekana kuthirika zaidi ya wale wasio na matamanio ya ngono.
 • Kuwa mwanamke, wanawake wana mrija mfupi wa kutoa mkojo kutoka katika kibofu ukilinganisha na wanaume. Kwa hiyo huwa ni rahisi kwa bakteria kufikia kibofu kwa wanawake, na kupata uambukizi.


Ugonjwa wa UTI unapotibiwa mapema, hupona kwa urahisi na hakuna madhara yeyote atapata mgonjwa. Lakini ugonjwa usipotibiwa na kuwa sugu madhara huweza kutokea. Madhara haya ni kama kuharibika kabisa kwa figo endapo mgonjwa ataishi na ugonjwa kwa muda mrefu bila kutibiwa. Athari hizi huwa ni zaidi kwa watoto ukilinganisha na watu wazima. Mwanamama mjamzito asiyetibiwa ugonjwa, anaweza kujifungua mtoto mwenye uzito mdogo au aliye njiti.

Mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa hufanyiwa vipimo vya kimaabara. Kwa uchunguzi zaidi bakteria huoteshwa katika maabara ili kuweza kugundua ni aina gani ya bakteria waliosababisha ugonjwa  na uchunguzi huu husaidia katika kuchagua tiba iliyo sahihi.

Vipimo vingine vya picha za ndani ya mwili vyaweza kutumika ili kuchunguza endapo mgonjwa amepata madhara katika njia ya mkojo. Vipimo hivi ni kama CT scan, ultrasound na X ray .

Pia mkojo waweza kuchunguzwa katika maabara kuangalia uwepo wa chembechembe za seli nyeupe za damu, seli nyekundu za damu au hata uwepo wa bakteria. Ni vyema mgonjwa anapotoa mkojo wa uchunguzi kuhakikisha mkojo huo hauingii vijimelea kutoka katika mazingira ya anapotolea mkojo huo.

Kamwe usitumie dawa bila ya kupata ushauri wa daktari na vipimo kuhakikisha aina ya ugonjwa. Baada ya vipimo onana na mfamasia kwa ajili ya dawa na ushauri kuhusu matumizi ya dawa.

Kwa ugonjwa usio sugu dawa kama Sulfamethoxazole-trimethoprim (Septrin) yaweza kutumika, Amoxiccilin+clavulanic acid (Augumentin), Nitrofurantoin na Ciprofloxacin zaweza kutumika kutibu ugonjwa.

Kwa kawaida dalili za ugonjwa hutoweka siku chache baada ya kuanza kutumia dawa, lakini hiyo siyo sababu ya kuacha kutumia dawa. Unaweza hitajika kutumia dawa zako kwa muda wa zaidi ya siku saba ili upone kabisa. Tumia kozi nzima ya antibiotiki kama ulivyoelekezwa na mfamasia wako ili kuhakikisha uambukizi unamalizika kabisa. Pia waweza kupewa dawa za kuondoa maumivu katika njia ya mkojo.

Mgonjwa anaweza kutibiwa pia kwa kuongezewa ostrogeni kama UTI inaambatana na ukomo wa hedhi (postmenopausal UTI)

Uambukizi ulio sugu hutibiwa baada ya uoteshaji wa bakteria katika maabara ili kuweza kugundua antibiotiki ifaayo zaidi. Mara nyingi mgonjwa huwa na kozi ndefu ya antibiotiki, na mara nyingine huitajika antibiotiki za kutumia kwa njia ya mishipa ya damu (Sindano)

Jinsi ya kujikinga na UTI
 • Epuka bidhaa za wanawake zenye antiseptiki, bidhaa hizi huuwa bakteria wenye faida(normal flora) na wanaoimarisha kinga ya mwili kwenye uke. Bidhaa hizi kama dochi,poda, sabuni, deodoranti zaweza kusababisha upate uambukizi kwa urahisi.
 • Jifute kuanzia mbele kwenda nyuma, hii ni baada ya haja ili kuepuka kuwapeleka bakteria wa tumboni katika mrija wa mkojo.
 • Kunywa vimiminika kwa wingi, hususani maji,hii husaidia kupata mkojo mwingi na kukojoa mara nyingi na kuwaondoa bakteria kutoka katika kibofu na kuepuka uambukizi.
 • Hakikisha bafu na choo vinafanyiwa usafi wa hali ya juu.
 • Hakikisha vyombo na vifaa vya bafuni na chooni ni visafi na maji yanayotumika pia ni safi. Waweza kutumia water guard kuhakikisha maji ya bafuni na chooni ni safi.
 • Matumizi ya tamponi yahitaji usafi wa hali ya juu, kwa kuwa waweza kuingiza katika uke bakteria wasababishao ugonjwa.
 • Wanawake waepuke nguo zinazobana, Nguo zisizobana husababisha uke kupata hewa na kuwa mkavu na kuepuka uvamizi wa bakteria. Epuka suruali za jeans zinazobana hususani katika maeneo yenye joto. Chagua nguo za ndani zenye fiba za asili, mfano nguo za pamba.

Jiunge na ST. AGGREY HEALTH COLLEGE

Thursday, 30 March 2017

FAHAMU FAIDA NYINGI ZA PAPAI.


Mpapai ambao kitaalam hujulikana kama Carica papaya, ni mti wenye tunda lenye virutubisho vingi ambao una asili na hulimwa na kustawi katika nchi za kitropiki. Mpapai  hukua hadi kufikia kimo cha mita 10. Mti huu huwa na makovu ambayo hutokana na majani ya mpapai yaliyoanguka unapokua.

Mpapai ni wenye asili ya bara la Amerika ya kati na kusini lakini badae mmea wa tunda hili ulisambaa katika visiwa vya Caribbean, Florida na Baadhi ya nchi za Afrika. Leo hii papai hulimwa katika nchi za India, Australia, Indonesia, Philippines, Malaysia, U.S na Hawaii.

 Mmea huu wenye jinsia tatu: jike, dume na jikedume(hermaphrodite). Mpapai dume huzalisha poleni (mbegu dume) lakini hauzai matunda. Mpapai jike hauwezi kuzaa matunda bila kurutubishwa na poleni kutoka mpapai dume. Mpapai dumejike hujitegemea na waweza kuzaa matunda wenyewe. Na mipapai yote inayolimwa kibiashara huwa ni dumejike. Tunda la papai lina kirutubisho cha beta carotene ambacho hulipa papai rangi nzuri ya chungwa ya kung'aa.

Virutubisho katika papai
Jedwali likionyesha kiasi cha virutubisho katika gramu 100 za papai.
Aina ya kirutubisho
Kirutubisho
Kiwango kilichopo
Vitamini
Vitamini A
135ug

Vitamini E
1   ug

Vitamini C
62 mg

Thiamine
0.0mg

Niacini
0.3mg

Vitamini B 6
0.0mg

Folate
38 ug
Madini
Kalshamu
24mg

Phosphorasi
5 mg

Magnesiamu
10mg

Potasiamu
257mg

Munyu (Sodium)
3mg

Chuma
0.1mg

Zinki
0.1mg

Shaba
0.0mg

Manganizi
0.0mg
Protini muhimu
TRP(Tryptophan)
8mg

THR(Threonine)
11mg

ILE(Isoleucine)
8 mg

LEU(Leucine)
16mg

LYS(Lysine)
25mg

MET(Methionine)
2 mg

CYS(Cysteine)
5 mg

PHE(Phenylalanine)
9 mg

TYR(Tyrosine)
5mg

VAL(Valine)
10 mg

 Matumizi ya matunda na mboga za majani yamekuwa yakihusishwa na kupungua kwa athari za kiafya zisababishwazo na mfumo mpya wa maisha. Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa kuongezeka kwa matumizi ya vyakula vitokanavyo na mimea kama papai hupunguza athari kama kuwa na uzito mkubwa, kisukari, magonjwa ya moyo na huboresha afya na kuongeza nishati mwilini. Zifuatazo ni baadhi ya faida zitokanazo na ulaji wa papai:

Tunda la papai lililowiva lina kiwango kikubwa cha Vitamini C (62mg) ukilinganisha na chungwa lenye kiwango cha 53mg katika gramu 100 za tunda. Tafiti zimeonyesha faida nyingi za vitamini C kama kuondoa sumu mwilini(sumu hizi hujulikana kama free radicals), kuimarisha kinga ya mwili na kujikinga na visababishi vya maumivu na uvimbe.

Papai hupunguza kiwango cha lehemu kwa kuwa lina Vitamini C na virutubisho vingine ambavyo huzuia kujijenga kwa lehemu katika mishipa ya damu ya ateri. Lehemu inapojikusanya kwa wingi katika ateri, mishipa hii ya damu huwa na njia nyembamba au kuziba na kusababisha kuongezeka shinikizo la damu na hata shambulizi la moyo.

Tunda hili husaidia kupunguza uzito wa mwili, papai lina fiba (nyuzi lishe) ambazo husaidia kupunguza uzito, unapokula tunda hili, fiba husababisha kujisikia umeshiba kwa hiyo mtu hupunguza kiasi cha chakula chenye nishati nyingi ambapo hupelekea kupunguza uzito wa mwili.

Afya njema ya macho hupatikana kwa kula tunda hili. Papai lina kiwango kikubwa cha Vitamini A na vitutubisho vingine kama Beta carotene ambavyo husaidia kuiweka katika hali ya afya njema ya ngozi utando ya macho, na kuzuia kudhurika kwa macho. Pia vitamini A huzuia kuharibika sehemu ya macho inayohusika na kuona kutokana na umri mkubwa na kutuepusha matatizo ya kuona.

Katika utafiti mmoja uliochapishwa katika jarida la magonjwa ya viungo(arthritis) ulionyesha kuwa, watu wanaokula vyakula vyenye kiwango kidogo cha vitamini C walikuwa katika hatari mara tatu zaidi ya kupata magonjwa ya viungo. Kula papai ni muhimu kwa afya ya mifupa yako kwa kuwa husaidia kuondoa visababishi vya uvimbe na maumivu pia lina vitamini C kwa wingi ambayo hutukinga na aina nyingi za magonjwa ya viungo.
Papai husaidia kuboresha mmeng'enyo, katika zama hizi, haikwepeki kula vyakula ambavyo huathiri mmeng'enyo na mfumo wa chakula. Mfano tunapokula vyakula vyenye mafuta na chumvi kwa wingi katika migahawa (junk food). Kula papai kutarekebisha mfumo kutokana na kuwepo kwa kimeng'enyo kijulikanacho kama papain pamoja na fiba kwa wingi ambazo husaidia kuboresha mmeng'enyo na kuimarisha afya yako.

Kuimarika kwa kinga ya mwili husaidia kujikinga na nyingi za magonjwa. Papai moja laweza kukuongezea kiasi kikubwa cha vitamini C inayohitajika mwilini kwa siku na vitamini hii inahusika katika kukutengenezea kinga imara mwilini.

Ingawa papai ni tamu, lakini lina kiwango kidogo cha sukari .Papai ni zuri kwa wale wenye kisukari kwa kuwa lina  vitamini na virutubisho ambavyo huwakinga wenye kisukari wasipate magonjwa ya moyo. Pia wasio na kisukari ni vyema kula papai ili kuweza kujiepusha na maradhi hayo yatishiayo maisha ya binadamu.

Wengi wetu hatupendi kuuzeeka, tungependa tuendelee kubaki katika hali ya ujana, lakini hakuna hata mmoja aliyefanikiwa. Papai hupunguza kasi ya kuzeeka kwa uwepo wa Vitamini C kwa wingi, viondoa sumu(antioxidants) pia kirutubisho cha beta carotene ambavyo hulinda ngozi zetu dhidi ya sumu (free radical) ambazo husababisha makunyanzi ya ngozi na hali nyingine za kuzeeka.

Mbali na kuiweka ngozi katika hali ya afya njema, papai pia husaidia ukuaji wa njwele na kuwa zenye afya, Vitamini A husaidia katika utengenezaji wa Sebum, kemikali ya kibiolojia ambayo huzifanya nywele zetu kuwa nyororo, imara na za kung'aa. Virutubisho katika tunda hili huzuia pia kunyonyoka kwa nywele.Mbali na kusaidia katika ukuaji wa nywele imara, inadhaniwa kuwa papai husaidia pia kuzuia nywele zisiwe nyembamba na kuzuia kukatika.

Uwepo wa viondoa sumu katika papai, husaidia kutukinga na maradhi ya saratani. Katika utafiti mmoja uliofanyika katika chuo kikuu cha Harvard katika kitivo cha afya ulionyesha kuwa, beta carotene katika papai huzuia kukua kwa saratani ya tezi dume na saratani ya utumbo mkubwa.

Mbali na vitamini na protini muhimu zilizopo katika tunda hili, pia kuna aina tofauti za madini(tazama jedwali) muhimu yanayohitajika mwilini kufanya na kurekebisha kazi mbalimbali za mwili. Faida nyinginezo mbali na tulizoziona awali za ulaji wa papai ni pamoja kuondoa msongo wa mawazo, kusaidia kupunguza maumivu ya hedhi, kupunguza hatari ya kupata pumu na husaidia ngozi au majeraha kupona haraka.

Jiunge na ST. AGGREY HEALTH COLLEGE-MBEYA